21 Aprili 2025 - 22:59
Source: Parstoday
IRGC kuzindua manowari mpya kama za US, au bora zaidi

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Admeli Alireza Tangsiri amesema yumkini SEPAH ikazindua manowari mpya ambazo muundo wake unashabihiana au utakuwa bora zaidi kuliko wa Marekani.

Akizungumza katika kipindi cha televisheni ya IRIB, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la IRGC ametoa mukhtasari wa mafanikio ya kijeshi ya kikosi hicho cha majini cha IRGC katika miaka ya hivi karibuni.

Kamanda Tangsiri amesema: Jeshi la Wanamaji la IRGC limetengeneza aina mbalimbali za makombora, ndege zisizo na rubani, na nyambizi, na Wizara ya Ulinzi kwa ushirikiano na Shirika la Usaidizi wa Vikosi vya Wanajeshi pia imezalisha nyambizi bora za kisasa.

Akizungumzia uundaji wa meli ya kubeba ndege zisizo na rubani ya IRGC Shahid Bagheri, Admeli Tangsiri amesema, "Meli ya Shahid Bagheri ni meli ya matumizi mbalimbali na ni kituo cha kijeshi cha majini; chombo hiki kinaweza kubeba mifumo miwili ya kurusha makombora, ambayo ni meli 14 za kurusha makombora."

"Tumeunda meli ambayo ni bora zaidi kuliko miundo sawa ya Kimarekani, na katika wakati mwafaka, tutaizindua," Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la IRGC amesema hayo alipokuwa akizungumza kuhusu meli mpya za kikosi hicho.

Alipoulizwa kuhusu makabiliano ya Iran na Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi, ameeleza bayana kuwa, "Leo, Marekani haiwezi kushambulia meli zetu za mafuta, na ikiwa itafanya hivyo, tutakabiliana nayo."

"Wamarekani hawawezi kutukabili katika Ghuba ya Uajemi kwa sababu tuna uwezo wa kupambana nao," amesisitiza Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha